Read more
Duka la Mangi ni nini?
Duka la Mangi namaanisha yale maduka ya mtaani ambayo huuza bidhaa mchanganyiko mfano soda, pipi, biskuti, majani ya chai, sukari, chumvi, mafuta pamoja na vyakula kama mchele, sembe, ngano, maharage n.k.
Maduka haya ni mengi sana kila kona ya mtaa na mara nyingi ndio tunapopata mahitaji yetu ya kila siku kwa uharaka na wepesi na bei nafuu sana.
Leo nitakufundisha mambo muhimu ya kuzingatia kama unataka kufungua biashara hii ili uweze kujiingizia kipato.
1. Eneo
Ili uweze kufanikiwa kwenye biashara hii hakikisha unatafuta eneo zuri la mtaani ambapo kuna muingiliano wa watu na makazi ya watu maana hao ndio watakuwa wateja wako wa kwanza na wa kudumu ukiachilia wapita njia.
Zingatia:Eneo ambalo lipo kwenye kona linaweza kufaa zaidi, hapo utatega wateja wanaotoka engo zote.
2. Aina za Bidhaa
Hili ni jambo muhimu sana naenda kuelezea na wengi wao ambao wanaanza biashara hii wanakuwa hawalijui au wanalipuuzia, bidhaa gani utaweka kwenye maduka ya hii ni muhimu sana kujua, kitu cha kwanza ambacho hutakiwi kukosa ni vyakula kama unga wa sembe, mchele, maharage, mafuta ya kula, sukari, majani ya chai, mayai, pia kuwa na friji ili uweze kuuza vinywaji baridi na mwisho usisahau vocha hii ni muhimu kwa ajili ya kuchangamsha duka na kuvutia wateja wengi zaidi, baada ya hivyo ndo enndelea na hizo bidhaa zingine ambazo najua unazifahamu kama pipi, biskuti na nyingine nyingi kulingana na mtaji utakaokuwa umeanza nao au unao.
3. Kauli
Mbali na kuwa na eneo zuri na bidhaa nzuri kitu kingine cha kuzingatia ni kauli kwa wateja, hii itakuongezea au kukupotezea wateja kama hautakuwa makini nalo. Jitahidi uwe na lugha nzuri ila usiruhusu wateja wakupande kichwani na kukopesha hovyohovyo si ajabu utafilisika na kufunga biashara hivyo kuwa mkarimu na karibisha wateja vizuri lakini pia kuwe na mipaka ya biashara.
Jifunze kusema asante pindi mteja anaponunua dukani kwako hii itakupeleka mbali na kukutofautisha na wauzaji wengine.
4. Sehemu Unapochukulia Mzigo
Hii ni biashara ambayo unanunua mzigo kwa bei ya jumla na kuuza kwa rejareja, sasa ili uweze kupata faida nzuri utatakiwa kufanya utafiti mtaani kwako nani anauza bidhaa kwa bei rafiki kuliko wengine na uwe unachukua hapo, kwenye hili kuwa makini sana maana wauzaji wa jumla ni wengi na ushindani ni mkubwa hivyo hili halisumbui.
Itaendelea.......
0 Reviews